31 Julai 2023 - 17:05
Uturuki yafunga ofisi ya kundi la Ikhwanul Muslim la Misri

Viongozi wa kundi la Ikhwanul Muslimin la Misri wanaoishi nchini Uturuki wamekuwa chini ya shinikizo ya serikali ya Ankara tangu mwezi Machi mwaka huu, wakati maafisa wa usalama wa Uturuki na Misri walipokuwa katika mazungumzo ya kurejesha uhusiano wa kawaida baina ya nchi hizo mbili.

Shirika la habari la Tasnim limenukuu taarifa ya jarida la Yeni Asia ikisema kuwa, serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan hivi sasa inalipa umuhimu mkubwa suala la kurejesha uhusiano na Misri, na hivi sasa imeamua kuzifunga ofisi za Makao Makuu ya Ikhwanul Muslimin ya Misri nchini Uturuki.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, tangu mwezi Machi mwaka huu, wakati maafisa wa usalama wa nchi hizo mbili walipokuwa katika mazungumzo, viongozi wa Ikhwanul Muslimin ya Misri wanaoishi Uturuki wamekuwa chini ya shinikizo ya serikali ya Ankara kiasi kwamba hata vyombo vyao vya habari vimeamriwa kutotangaza chochote cha kukosoa utendaji wa serikali ya Misri.

Mashinikizo hayo yameendelea hadi mwezi huu, ambapo habari zinasema kuwa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan imeamua kuzifunga ofisi kuu za Ikhwanul Muslimin ya Misri nchini Uturuki. 

Uhusiano kati ya Uturuki na Misri ulikatika kikamilifu tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi nchini Misri yaliyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Sisi dhidi ya Mohammed Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Misri mwaka 2013. Nchi mbili za Uturuki na Misri zimepitia kipindi Kizito cha mvutano hasa baada ya Mohammad Morsi kufa gerezani kiasi kwamba Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alimwita Morsi kuwa ni shahidi aliyeuliwa kidhulma na serikali ya Rais Abdel Fattah el Sisi.

Hivi sasa lakini mambo yamebadilika kikamilifu. Nchi mbili za Misri na Uturuki zimerejesha hata uhusiano wao wa kidiplomasia. Matukio mbalimbali yaliyotokea hivi sasa kisiasa na kikanda katika eneo la Bahari ya Mediterania ya Mashariki na hali mbaya ya kiuchumi ya Misri hasa baada ya uvonjwa wa UVIKO-19 na vita vya Ukraine na pia matetemeko makubwa ya ardhi ya hivi karibuni huko Uturuki na kaskazini mwa Syria, yamebadilisha sana misimamo ya Ankara na Cairo. Baada ya matetemeko hayo ya ardhi, Sameh al-Shakri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri alielekea nchini Uturuki na kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi.

Wakati wa Kombe la Dunia la Qatar, Erdoğan na El-Sisi, marais wa Uturuki na Misri, walikutana ana kwa ana katika mkutano wao wa kwanza baada ya mvutano wa muongo mzima. Mazungumzo hayo ya ana kwa ana yalionesha azma ya nchi hizo mbili kufufua uhusiano wao.

Baada ya hapo Rais wa Misri Abdel Fattah el Sisi alitembelea Uturuki tarehe 27 mwezi huu, na lengo la safari hiyo lilitajwa kuwa ni kutanua uhusiano wa pande mbili na kukagua maendeleo ya kikanda.

342/